2 Chronicles 1:3-12

3 aNaye Solomoni na kusanyiko lote wakakwea mpaka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kwa kuwa huko ndiko Hema la Kukutania la Mungu lilipokuwa, ambalo Mose mtumishi wa Bwana alikuwa amelitengeneza huko jangwani. 4 bBasi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu mpaka mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu. 5 cLakini yale madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza yalikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani ya Bwana Mungu, hivyo Solomoni na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko. 6 dSolomoni akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za Bwana katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu 1,000 za sadaka za kuteketezwa juu yake.

7 eUsiku ule Mungu akamtokea Solomoni na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.”

8 fSolomoni akamjibu Mungu, “Umemwonyesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake. 9 gSasa, Bwana Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi. 10 hNakuomba unipe mimi hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?”

11 iMungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, 12 jkwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”

Copyright information for SwhNEN